Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amezindua kampeni ya kuhamasisha utoaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari Mkoani humo kwa kutumia vyakula vya asili vinavyopatikana kwenye maeneo husika.
Dkt. Mussa amezindua kampeni hiyo leo Januari 19, 2024 katika viwanja vya shule ya msingi Mtombozi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kwa lengo la kuhamasisha wazazi na walezi kuchangia upatikanaji wa chakula cha mchana kwa wanafunzi Mkoani humo.
Dkt.Mussa amesema Mkoa wa Morogoro umebarikiwa kuwa na aina mbalimbali za vyakula vya asili vikiwemo mashelisheli, mihogo, Viazi vitamu na ndizi huku hivyo haoni sababu ya wanafunzi kukosa chakula mchana na kuwataka wazazi kwa kushirikiana na Walimu kufanikisha upatikanaji wa vyakula hivyo kulingana na maeneo husika.
“...kuja kwangu leo hapa ni kuanzisha hii kampeni, si kwa hapa tu lakini kwa Halmashauri nzima na Morogoro nzima lazima tukubali kutumia vyakula vyetu vya asili tulivyokuwa navyo...” amesema Dkt. Mussa.
Aidha, Dkt. Mussa ameeleza kuwa kukosekana kwa chakula shuleni kuna sababisha utoro na kushuka kwa ufaulu wa wanafunzi, hivyo ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kuhakikisha kuwa inapanda miche ya mashelisheli angalau miche miwili kwa kila shule za Wilayani humo.
Naye Afisa Lishe Mkoa wa Morogoro Bi. Salome Magembe amewashauri wazazi na walezi kuzingatia makundi matano ya vyakula Vikiwemo vyakula vya protini, wanga, Vitamini, mafuta na mboga mboga ili kupata mlo kamili kwa ajili ya kuboresha afya.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Ndg. Patrick Gwivaha amemshukuru Katibu Tawala kwa kuanzisha na kutulia mkazo kampeni hiyo ambayo itasaidia kupandisha kiwango cha ufaulu katika Halmashauri na kumhakikishia utekelezaji mzuri wa maagizo aliyoyatoa.
Katika kuhamasisha kampeni hiyo Dkt. Mussa ameahidi kuichangia shule ya msingi Mtombozi dagaa kilo 100 kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.