Waziri mkuu wa Jamhuri ya muungano ya Tanzania ametembelea eneo unapojengwa mradi mkubwa wa kufua umeme unaotokana na maporomoko ya maji ya Mto Rufiji maarufu kama Stiglers gorge.
Waziri Mkuu ametembelea eneo hilo, alipokuwa katika ziara ya siku mbili Mkoani Morogoro na kuamua kutembelea na kujionea mwenyewe maandalizi ya ujenzi wa Mradi huo ambao upo mpakani mwa Wilaya ya Morogoro Mkoani Morogoro na Wilaya ya Rufiji Mkoani Pwani.
Baada ya kutembelea na kupewa maelezo ya maandalizi ya ujenzi mradi huo kuwa yamefikia asilimia 80 alieleza kuwa mradi huo pamoja na malengo mengine unalenga kudhibiti uharibifu wa mazingira na siyo kuharibu mazingira kama ambavyo baadhi ya watu wanavyosema.
Awali waziri mkuu alipata maelezo ya maendeleo ya mradi toka kwa waziri wa nishati na madini Dkt.Medard Kalemani ambaye alisema kuwa:- Ujenzi wa barabara na ukarabati wa madaraja kufika eneo la mradi ( barabara ya kutoka Kibiti hadi na eneo la mradi na barabara ya kutoka Ubena Zomozi hadi eneo la mradi) umefikia asilimia 88.
Kazi ya kupeleka umeme katika eneo la mradi ( kV 33) kutoka Msamvu Morogoro kwa umbali wa kilometa 69. 2 imekamilika na kinachofanyika sasa ni kutandaza nguzo katika eneo la mradi.
Kazi ya kujenga miundombinu ya maji kwa ajili ya wafanyakazi watakaokuwa katika eneo la mradi imekamilika kwa asilimia 100.
Kazi ya kujenga na kupanua reli katika eneo la Fuga inatarajiwa kukamilika mwezi huu.
Kazi ya kukuza mawasiliano katika eneo la hifadhi inaendelea.
Katika taarifa yake Mh waziri wa nishati alisisitiza kuwa Matarajio ni kuwa shughuli zote zitakamilika ifikapo tarehe 10 mwezi huu.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa katika eneo la mradi wa umeme wa Rufiji (2100) alikagua eneo la mradi na pia alikagua ujenzi wa kituo cha reli ya Tazara eneo la Fuga kitakachotumika kushusha mizigo wakati wa utekelezaji wa mradi huo wa umeme.
Mvuha Area, Mvuha - Magogoni Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.