
Shirikisho la Uhifadhi wa Mazingira Asilia Duniani (IUCN) leo Oktoba 3, 2025 wametambulisha Mradi wa RESOLVE NbS katika ngazi ya Halmashauri, pamoja na mmoja wa mbia katika utekelezaji ambaye ni CARE.
Mradi huo wa RESOLVE NbS (SULUHISHO) ni mradi wa Uhifadhi wa Mazingira kwa njia za Asili, ambapo vijiji vinne vya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro vitanufaika. Vijiji hivyo ni Kisarawe na Milawilila vilivyopo Kata ya Tawa, pamoja na Amini na Kalundwa vilivyopo Kata ya Kinole.

Ukiwa unakwenda sambamba na kauli mbiu ya UHAI, USTAHIMILIVU na MAENDELEO, Mradi wa Suluhisho utakuwa wa miaka mitatu (2025–2027) na utajikita zaidi katika shughuli za; -
1. Kuwezesha wadau mbalimbali, hususan sekta binafsi, katika namna bora ya kupanga na kutekeleza masuluhisho asilia;
2. Kuimarisha uwezo wa maafisa wa halmashauri juu ya kupanga na kuingiza vipaumbele vya kuhimili mabadiliko ya tabianchi kwenye mipango na bajeti;
3. Kuhamasisha jamii juu ya utekelezaji wa kilimo mseto na kilimo bioanuai kwa kupitia mashamba darasa;
4. Kutengeneza au kuboresha mipango ya matumizi bora ya ardhi kutokana na kiwango cha uhitaji ukilinganisha na vijiji vingine vya mradi;
5. Kurejesha ikolojia za misitu, ardhi na mito zilizoharibiwa;
6. Kuboresha uwezo na mifumo ya jamii kwenye kuweka na kukopa (VSLA);
6. Kuboresha mifumo ya uuzaji wa mazao kwa kutumia vyama vya ushirika (AMCOS); na
7. Kutengeneza Mpango Mkakati wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi na kukabiliana na maafa katika ngazi ya Wilaya.
Lengo kuu ni kuimarisha ustahimilivu wa watu na rasilimali dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutumia masuluhisho asilia.

Utekelezaji wa shughuli tajwa za Mradi, pamoja na nyinginezo, utahusisha wabia mbalimbali ambao ni CARE, WWF, EAMCEF, CAN na CEO Round Table (CEOrt), ambapo jumla ya Dola za Kimarekani milioni 5.3 zinatarajiwa kutumika.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.