Naibu Waziri OR-TAMISEMI (Afya) Mhe. Dkt. Festo John Dugange amefanya Ziara ya siku moja kukagua miradi ya afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ambapo awali alikuwa atembelee Zahanati ya Kibuko ambayo ilianzishwa kwa nguvu za wananchi lakini pia Hospitali ya Wilaya inayoendelea kujengwa (Mvuha), lakini Mhe. Naibu Waziri alifanikiwa kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Juni 19, 2021.
Naibu Waziri OR-TAMISEMI (Afya) Mhe. Dkt. Festo J. Dugange ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kumaliza ujenzi wa Wodi 3 za watoto, wanawake na wanaume ifikapo Julai 19, 2021 kama ambavyo Mhandisi wa Halmashauri ameeleza kwamba ifikapo Julai 19 majengo hayo yatakuwa yamekamilika.
"Tumegundua kwamba mmechelewa kukamilisha miradi kwa Kadri ya maelekezo ya Serikali na mumetoa maelezo yenu lakini moja tu zuri ambalo mumeniahidi ni kwamba ifikapo tarehe 19 ya mwezi wa saba kwamba majengo haya yote yatakuwa yamekamilika. Na mimi nawaelekeza muhakikishe usiku na mchana mnapambana kwa kuzingatia ubora, viwango na thamani ya fedha Wodi hizi zikamilike kama ambavyo mumesema wenyewe."
Katika hatua nyingine Mhe. Dkt. Festo J. Dugange amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kwa usimamizi mzuri wa miradi ya afya licha ya kuwa na watumishi wachache hasa kwenye idara ya ujenzi.
"Niwapongeze sana kwa maana ya ubora wa majengo kwa kweli ubora wa majengo unaona kabisa yana thamani ya fedha ambayo mpaka sasa imeshatumika, mumejenga kwa kuzingatia viwango na unadhifu mzuri lakini usimamizi mzuri pamoja ni kwamba kuna engineer (Mhandisi) mmoja tu na miradi ni mingi sana lakini kwa kweli Mkurugenzi hongera sana mumejitahidi sana kama Halmashauri kusimamia hii miradi."
Aidha akisoma taarifa ya idara ya afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Mkurugenzi Mtendaji Bi. Rehema S. Bwasi amesema, "Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2018/2019 hadi sasa tumepokea fedha kutoka Serikali kuu kiasi cha Shilingi Bilioni tano na Milioni Mia moja na hamsini kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya 6, Hospitali ya Wilaya pamoja na Zahanati 7"
Lakini pia kwenye taarifa hiyo Bi. Rehema S. Bwasi ametoa taarifa ya kupungua kwa vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga toka 2018 hadi sasa.
Akiongea na timu hiyo ya wakuu wa idara na vitengo ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Mhe. Dkt. Festo Dugange amesema, "Mmeendelea kwa kiasi kikubwa sana kupunguza kasi ya vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga, nikiangalia mmetaja kwa miaka mfululizo 2018, 2019, 2020 tunaona kabisa ile trend ni ya kushuka chini. Kwa hiyo niwapongeze sana Dkt. Manyerere na timu yako ya CHMT"
Aidha Mhe. Dkt. Festo Dugange amezungumzia kuhusu CHF iliyoboreshwa na kusema, "Jambo kubwa katika CHF ni Uhamasishaji na ili uhamasishe vizuri kwenye CHF ni lazima Dawa zipatikane ili wale uliowasajiri awamu ya Kwanza wakawe mabalozi wazuri kuwasemea kwa jamii kwamba CHF inafaa."
Katika hatua nyingine Mhe. Dkt. Festo Dugange amewaambia timu hiyo ya wakuu wa idara na vitengo kwamba Serikali inatambua na kuthamini kazi wanayoifanya katika kuhudumia Wananchi.
#KAZI IENDELEE
Mvuha Area, Mvuha - Magogoni Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.