Serikali imesema kuwa mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya Sh bilioni 553.39 zimekusanywa kati ya Sh bilioni 687.31 ambazo ni sawa na asilimia 81 ya lengo ambalo halmashauri zote nchini ilijiwekea.
Aidha, Dodoma imeongoza katika ukusanyaji wa mapato kwa upande wa majiji na mikoa ambapo Halmashauri ya Mji Geita ikiwa kinara katika mlinganisho wa kiasilimia kwa Mamlaka zote za Serikali za Mitaa bila ya kujali hadhi huku halmashauri ya Mbinga ikishika mkia.
Akitangaza makusanyo kwa halmashauri zilizofanya vizuri na vibaya, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo alisema: " TAMISEMI imekuwa ikifuatilia ukusanyaji wa mapato katika halmashauri zake ili kuweza kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri zote nchini.
" Baada ya kumaliza zoezi la usuluhishi wa kibenki takwimu zinaonyesha kwamba kwa mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya shilingi 553,390,075,912 zimekusanywa kati ya shilingi 687,306,661,000 ambazo ni sawa na asilimia 81 ya lengo."
Jafo alisema kwa upande wa Majiji, Jiji la Dodoma limekuwa la kwanza kati ya majiji sita likiwa limekusanya Sh bilioni 25.06 kati ya Sh bilioni 19.33 ambayo ni sawa na asilimia 130 ya lengo wakati Jiji la Mbeya limekuwa la mwisho kwa kukusanya kiasi cha Sh bilioni 7.82 kati ya Sh bilioni 11.0, sawa na asilimia 71.
Dar es Salaam ni ya pili ikiwa imekusanya Sh bilioni 15.67 kati ya makisio ya Sh bilioni 16.41 ambayo ni asilimia 95, Arusha ya tatu ikikusanya Sh bilioni 13.59 kati ya lengo la Sh bilioni 14.58, Mwanza imeshika nafasi ya nne ikikusanya Sh bilioni 10.47 kati ya malengo ya Sh bilioni 1.44, Tanga ikikusanya Sh bilioni 10.84 kati ya malengo ya Sh bilioni 14.03.
Jafo alisema Manispaa ya Iringa ndiyo ilikuwa ya kwanza kwa kukusanya Sh bilioni 4.28 kati ya Sh 4.17 ambayo sawa na asilimia 103 ikifuatiwa na Manispaa ya Temeke iliyokusanya Sh bilioni 29.41 kati ya lengo la kukusanya Sh bilioni 29.07 sawa na asilimia 101.
Alisema katika kundi hili, Manispaa ya Ilemela ilikuwa ya mwisho kwa kukusanya Sh bilioni 4.76 kati ya lengo la kukusanya Sh bilioni 11.75 sawa na asilimia 40.
Jafo alisema Halmashauri ya Mji wa Geita ndiyo ilikuwa ya kwanza kwa kukusanya Sh bilioni 6.86 kati ya lengo la kukusanya Sh bilioni 3.15 sawa na asilimia 218 ikifuatiwa na Halmashauri ya Mji wa Njombe iliyokusanya Sh bilioni 2.93 kati ya lengo la kukusanya Sh bilioni 2.40 sawa na asilimia 122.
Alisema Halmashauri ya Mji wa Nanyamba ni ya mwisho kwa kukusanya Sh bilioni 1.14 kati ya lengo la kukusanya Sh bilioni 2.11 sawa na asilimia 54.
Jafo alisema Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ilikuwa kinara kwa kukusanya Sh bilioni 3.09 kati ya Sh bilioni 1.87 sawa na asilimia 165 ikifuatiwa na Halmashauri ya Mpimbwe iliyokusanya Sh bilioni 1. 55 kati ya Sh milioni 956.84 sawa na asilimia 162.
Alisema halmashauri za wilaya zilizofanya vibaya zaidi ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga iliyokusanya asilimia 20, halmashauri ya Songea iliyokusanya asilimia 33, Halmashauri ya Rorya ilikusanya asilimia 37 na Halmashauri ya Siha iliyokusanya asilimia 39.
Aidha, Jafo alisema katika mlinganisho wa kiasilimia kwa Mamlaka zote za Serikali za Mitaa bila ya kujali hadhi zao, halmashauri tatu kinara kwa makusanyo kiasilimia ni Halmashauri ya Mji wa Geita ambayo imekusanya kwa asilimia 218, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha ambayo imekusanya kwa asilimia 165 na Halmashauri ya Mpimbwe iliyokusanya kwa asilimia 162 .
ASILIMIA YA MAKUSANYO YA MAPATO NDANI YA HALMASHAURI KWA MWAKA 2017-18.pdf
Mvuha Area, Mvuha - Magogoni Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.