Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wabia wa sukari ambao ni NSSF pamoja na Jeshi la Magereza kuhakikisha serikali inafikia malengo ya uzalishaji sukari kwa kiwango kinachotarajiwa kwa kuzalisha tani 485,000 ifikapo 2020 ikiwa ni mahitaji ya sukari ya majumbani kwani sasa serikali inatumia fedha nyingi kuagiza sukari nje ya nchi, hivyo njia pekee kufikia malengo hayo ni kuwa na shamba kubwa la miwa, kiwanda na mashine itakayokamua miwa hiyo ili kufanikisha upatikanaji wa sukari.
Majaliwa amesema kuwa kwa sasa kiwango kinachozalisha ni tani 345,000 hivyo ameitaka menejimenti mpya ya NSSF pamoja na bodi mpya ya Mkulazi kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza ambao ni wabia kutoka na mpango thabiti wa kusimamia mashamba ya Mkulazi 1 na 2 yaanze kazi mara moja kwa kuimarisha mifumo yote ya maji ili kuyakusanya yasaidie wakati wa kiangazi.
Aidha amewataka wakazi wa Kilosa na maeneo ya jirani kutumia fursa ya kilimo hicho cha miwa kujifunza na kulima kitaalam kwani vitendea kazi vipo, usimamizi na ushauri utapatikana kupitia wataalam watakaopatikana katika shamba hilo la miwa na kwamba miwa watakayolima itapeleka kiwandani na kuchakatwa jambo litakaloinua uchumi wa mtu mmoja mmoja
Sambamba na hayo Waziri Mkuu amewaagiza wakurugenzi wote nchini kuhakikisha maafisa kilimo wote nchini hawakai ofisini badala yake wasambae katika kata na vijiji yalipo mashamba ili kuwasaidia wakulima katika namna bora ya kulima kisasa ili waweze kupata tija kupitia kilimo na ametoa wito kwa watumishi wa umma kulima ili kujiongezea kipato kwani ardhi ya kutosha ipo.
Katika ziara yake Waziri Mkuu ameambata na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu Mh. Jenista Mhagama pamoja na Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Omary Mgumba.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.