Na Tajiri Kihemba.
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Loata Ole Sanare amefanya ziara katika Kijiji cha Mkono wa mara kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ambapo kuna mpaka unaotenganisha Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero ambao umekuwa na mgogoro wa muda mrefu.
Katika Ziara hiyo Mhe. Ole Sanare ameongozana na viongozi mbalimbali kutoka Halmashauri zote mbili na kupata fursa pia ya kufanya mkutano na Wananchi wa Vijiji viwili vilivyopakana vya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro na Mvomero.
"Ninaishukuru sana Timu ya ardhi ya Wilaya zote mbili za Morogoro na Mvomero wakiongozwa na Kamishina wa ardhi wa Kanda kwa kumaliza mgogoro huu wa mipaka. Mgogoro umeisha lakini tufuate utaratibu na Sheria zilizowekwa za kugawa ardhi." Amesema Mhe. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Aidha Mhe. Ole Sanare ameongezea kwa kusema "Natambua kuna watu wanajimilikisha ardhi maelfu ya hekari, wapeni salamu. Maeneo yatengwe kwa ajili ya shule, zahanati, maeneo ya kuzika lakini pia maeneo ya kuabudia na Serikali za Vijiji zihakikishe zinatenga maeneo hayo kwa kufuata utaratibu na Sheria."
Mhe. Ole Sanare pia amesema anatambua uwepo wa wazee wanaojifanya ndio wazee wa Vijiji na akimtaja Mzee Koka kuwa ni mmoja wa wazee waliojimilikisha eneo kubwa la ardhi na kunyang'anya wengine. Hivyo ameagiza wale wote wanaomiliki maeneo makubwa wajisalimishe katika Serikali za Vijiji na wathibitishe umiliki wao kwa kuonyesha nyalaka halali.
Mwisho Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Ole Sanare amewataka Wananchi kujitolea nguvu zao kuleta maendeleo katika Vijiji vyao na ameahidi kurudi tena kufanya harambee ya kuongeza madarasa shule iliyopo kijijini hapo.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.