Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa alikuwa mgeni katika zoezi la ugawaji kadi za bima ya afya kwa kaya masikini na watoto wanaoishi katika mazingira magumu zilizotolewa na Kikundi cha wanawake cha UMAKI kinachonufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Kikundi cha UMAKI ni kikundi cha wanawake wanaojishughulisha na ujasiliamali wa mama lishe ambao wamekuwa wakipatiwa mikopo na Halmashauri kwa ajili ya kujiinua kiuchumi na sasa wameweza kuwasaidia na wengine ambapo wanawasomesha watoto wanne wanaotoka katika mazingira magumu, watatu wakiwa shule ya Msingi na mmoja shule ya sekondari.
Lakini pia kikundi cha UMAKI kimefanya kitu kikubwa sana kwa jamii inayowazunguuka kwani wameweza kuwakatia bima ya afya ya Jamii (CHF) kaya zipatazo 13 zenye wanufaika 78 na sasa wanufaika hawa wanakwenda kupata matibabu katika kituo chochote kinachotoa huduma ya afya kwa kupitia kadi ya CHF iliyoboreshwa.
UMAKI kinakuwa kikundi cha pili kati ya vikundi vingi vinachofanya vizuri zaidi kupitia mikopo ya asilimia Kumi inayotolewa na Halmashauri yetu ya Wilaya ya Morogoro kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, lakini pia Kikundi cha BossKuku kilichopo katika Kijiji cha Mlilingwa katika Tarafa ya Ngerengere.
Hata hivyo kuna vikundi vingi vinafanya vizuri lakini BossKuku na Umaki ni mfano wa kuigwa zaidi, na hii inatoka na jitihada za makusudi zinazofanywa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Bi. Rehema S. Bwasi na wasaidizi wake kutoka idara ya maendeleo ya jamii ikiongozwa na Bi. Florence Mwambene kwa kuwajengea uwezo wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa namna gani wanaweza kujikwamua kiuchumi kwa kupitia mikopo hii.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.