Na Tajiri Kihemba.
Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Kalobelo ambae ni Mgeni rasmi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani kimkoa yaliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri Morogoro amekabidhi vyeti kwa wafanyakazi hodari toka Taasisi mbalimbali zilizopo ndani ya Mkoa wa Morogoro na kuhutubia hadhara ya Wafanyakazi na Wananchi waliofika uwanjani hapo.
Katika hotuba yake Mhandisi Emmanuel Kalobelo amesema, "Waajiri waweke mazingira wezeshi ya kuwepo kwa vyama vya Wafanyakazi na kuacha tabia ya kudhohofisha vyama vya Wafanyakazi na haki za Wafanyakazi kwani hiyo sio dhamira ya Serikali yetu, uzoefu unaonyesha kuwa pale ambapo kuna matawi ya vyama vya Wafanyakazi ambayo yanatimiza majukumu yake vizuri na menejimenti inatimiza wajibu wake ipasavyo, uhusiano wa kikazi huwa mzuri"
Mhandisi Emmanuel Kalobelo ameeleza zaidi kwa kusema, "hii husaidia kupunguza migogoro, kuepusha migomo na huongeza tija na ufanisi, matawi haya hutoa fursa ya majadiliano na mazungumzo Kati ya Wafanyakazi na waajiri, Uhuru wa Wafanyakazi kujiunga na vyama vya Wafanyakazi ipo kisheria na halina mjadala."
Katika hatua nyingine Mhandisi Emmanuel Kalobelo amesisitiza kuwa anaamini waajiri wa Mkoa wa Morogoro wengi ni wastaarabu na wanafuata Sheria, wale wachache wanaokiuka Sheria kwa makusudi wote anaomba apatiwe orodha ili aweze kufuatilia na kuhakikisha kwamba Sheria hiyo inasimamiwa na inafanya Kazi katika maeneo hayo.
Aidha akizungumzia swala la migogoro sehemu za kazi, Mhandisi Emmanuel Kalobelo amesema, "utatuzi wa migogoro ya kikazi kama mlivyozungumzia kwenye risala yenu, Serikali itawasiliana na wadau husika kwenye Wizara ili kuona uwezekano wa kufungua Ofisi ya idara ya Kazi kwenye maeneo yenye Wafanyakazi wengi katika Mkoa wetu wa Morogoro ili Wafanyakazi waweze kupata huduma hiyo kwa ukaribu."
Kuhusu ucheleweshwaji wa kesi za Wafanyakazi Mhandisi Kalobelo amesema, "Serikali itaendelea kuwawezesha majaji wa Mahakama kuu mara kwa mara kuamua kesi hizo, sambamba na hilo Serikali ipo hatua za mwisho kufungua Ofisi ya jaji mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya Morogoro."
Mhandisi Emmanuel Kalobelo pia ameiagiza Ofisi ya Afisa Kazi Mkoa wa Morogoro ihakikishe kaguzi za mara kwa mara kwenye maeneo ya Kazi zinafanyika ili kujiridhisha kama mikataba ya Wafanyakazi inazingatia sheria.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.