Na. Tajiri Kihemba, MOROGORO DC.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya imedhamiria kukusanya taarifa za vifo vinavyotokea katika jamii ili kurahisisha upangaji wa mipango mbalimbali ya kimaendeleo kwa kutumia takwimu halisi za vizazi na vifo.
Hayo yamejidhihirisha leo Aprili 5, 2022 kupitia Mkutano maalumu wa Uhamasishaji juu ya Ukusanyaji wa taarifa za vifo vinavyotokea katika jamii ulioandaliwa na wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro wakihusisha Madiwani na Maafisa Watendaji wa Kata Kumi za Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Akielezea lengo la Mkutano huo Afisa Takwimu kutoka Wizara ya Afya, Ndugu Gisbert Msigwa amesema lengo ni kuwajulisha viongozi wa Mikoa, Halmashauri, Kata, Mitaa na Vijiji juu ya kuanza kwa zoezi la kufanya mahojiano ya vifo vinavyotokea katika jamii, kuelezea faida za kukusanya taarifa za vifo pamoja na kuelezea masuala mbalimbali yanayohusiana na mahojiano ya vifo vinavyotokea katika jamii.
Akizungumza kwa niaba ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Mhe. Robe Zongo Robe amesema anaishukuru Serikali ya Rais @samia_suluhu_hassan kwa juhudi za makusudi za kuleta maendeleo katika Nchi yetu na kuahidi kutoa ushirikiano katika kuelimisha na kuhamasisha Wananchi kutoa taarifa za vifo kwa Maafisa Watendaji wa Kata ili kuwezesha takwimu hizo kutumika katika mipango mbalimbali ya Serikali.
Aidha, Maafisa Watendaji wa Kata wamepewa mamlaka na RITA ya kutoa vibali maalumu vya mazishi katika maeneo yao na muda mchache ujao Maafisa Watendaji hao watapatiwa mafunzo ya mfumo, hivyo vifo vyote vitakuwa vikirekodiwa katika mfumo maalumu ili kurahisisha upatikanaji wa takwimu hizo muhimu.
#SerikaliYaAwamuYaSitaKazini #morodcmpya
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.