Shirika lisilo la Serikali la maendeleo E-MAC limetambulisha mradi wa 'FEED THE FUTURE TANZANIA IMARISHA SEKTA BINAFSI' katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.Kikao Cha kutambulisha mradi huo kimefanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya Morogoro ambapo mradi umetambulishwa kwa wataalamu na wakuu wa idara mbalimbali za Halmashauri ili kupata ushirikiano katika utekelezaji.
Akiongea kwa niaba ya shirika hilo, Msimamizi wa Mradi Bi. Naomi Lukumay ameeleza lengo la mradi katika Halmashauri na baadhi ya maeneo kuwa ni kusaidia vijana wajasiriamali binafsi."Lengo la mradi huu ni kusaidia vijana waliopo kwenye sekta ya kilimo kutambua fursa na kuzitumia yaani 'access to and use of financial and market resources '...." alisema Bi. Naomi
Mradi huu wenye kauli mbiu Tanzania Imarisha Sekta Binafsi unalenga kuwajengea uwezo vijana wajasiriamali zaidi ya 200 wa sekta binafsi kuelewa upatikanaji na matumizi ya huduma za biashara na fedha pamoja na fursa zinazolingana na mahitaji, uwezo na matarajio yao.
Aidha Bi. Naomi ameeleza kuwa Mradi huu ni wa miaka mine, ulioanza utekelezaji wake mnamo mwezi Mei 2022 na unatarajia kuongeza uelewa wa vijana juu ya sera, sheria na miongozo ihusuyo uchumi wao pamoja na kufahamu umuhimu wa kusajili biashara zao, kupata ujuzi wa jinsi ya usindikaji wa mazao, kupata masoko ya uhakika ya bidhaa wanazozalisha, kuongeza mauzo pamoja na kuongeza ujuzi juu ya elimu ya kilimo endelevu na ushiriki kwenye mijadala ya sera.Bi. Naomi amefafanua kuwa, vijana watapaswa kuchangia asilimia 30 ya gharama ya vifaa wanavyovihitaji katika biashara zao na mradi utawafadhili kwa asilimia 70 ili waweze kufikia malengo yao katika kujiimarisha kiuchumi kupitia sekta binafsi kwa upande wa biashara na kilimo.
Nae Mratibu wa mradi Ndg. Samweli Luhaga ameshukuru kwa ushirikiano walioupata kutoka kwa uongozi wa Halmashauri na kuomba uendelezwe kwa manufaa ya vijana katika kuimarisha sekta binafsi haswa kwa vijana wajasiriamali kwa upande wa kilimo.
Bw. Chesco Lwaduka Kwa niaba ya Mkurugenzi amelitaka shirika hilo kutimiza malengo na kusimamia kanuni na taratibu kipindi chote cha utekelezaji wa mradi.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.