Na. Andrew Chimesela – Morogoro
Halmashauri Mkoani Morogoro zimetakiwa kutenga bajeti kwa kuajiri Maafisa Ustawi wa Jamii lengo ni kuongeza watumishi wa Kada hiyo ili kuboresha utoaji wa huduma na kutatua changamoto zinazoikabili jamii katika Wilaya husika.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Frank Jacob wakati akizifungua kikao kazi cha siku mbili kwa Maafisa Ustawi wa jamii kutoka Halmashauri za Mkoa wa Morogoro kilicholenga Maafisa hao kubadilishana uzoefu katika utendaji kazi wa Sekta hiyo.
Dkt. Frank amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Morogoro kuona umuhimu wa kuongeza idadi ya watumishi katika kada hiyo kama ambavyo hufanyika katika kada nyingine za utumishi ikiwemo Afya, Elimu pamoja na Kada Nyingine.
“Kuna changamoto nyingi katika jamii, lakini zaidi ya asilimia 75 ya changamoto hizo haziripotiwi katika sehemu husika kutokana na wananchi kukosa uwezo wa kuwafikia maafisa ustawi wa jamii kwa kuwa idadi yao ni ndogo hivyo kulazimika kumaliza changamoto zao kienyeji”, alisema Dkt. Frank.
Aidha, Dkt. Frank amewataka maafisa Ustawi jamii Mkoani humo kujenga mazoea ya kushirikiana zaidi na jamii ili wawe karibu na changamoto zinazojitokeza ndani ya jamii na kuharakisha kutatua badala ya kukaa Ofisini huku akiziomba halmashauri kuwawezesha kifedha na vitendea kazi vingine maafisa ustawi jamii hao ili kufanikisha wajibu wao.
Kuhusu vitendo vya unyanyasaji kwa watoto Dkt. Frank amesema vitendo hivyo bado vipo ndani ya Jamii ambapo takwimu zinaonesha kwa kila watoto wakike watatu mmoja amefanyiwa vitendo hivyo akiwa chini ya umri wa miaka 18 na kwa upande wa watoto wakiume kila watoto saba mmoja amefanyiwa vitendo hivyo akiwa na umri chini ya miaka 18.
Kutokana na hali hiyo Dkt. Frank amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii katika kikao hicho kuhakikisha wanajadili kwa kina namna bora ya kushughulikia matatizo hayo ili watoto wanaoathirika na majanga hayo wapate haki yao kisheria na watuhumiwa wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Kwa upande wake Jesca Kagunila ambaye ni Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Morogoro amebainisha lengo la kikao hicho cha siku mbili kuwa kina lenga kuwajengea uwezo Maafisa Ustawi wa Jamii wote wa Mkoa wa Morogoro kwa njia ya kubadilishana uzoefu na kupanga mikakati katika kutatua changamoto zinazoukabili Mkoa ndani ya Jamii.
Huku mwakilishi kutoka Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bi. Subistia Kabudi ambae pia ni Mratibu wa masuala ya ulinzi na usalama kwa mtoto, amesema Maafisa Ustawi wa jamii wana wajibu wa kutoa huduma kwa Jamii kwa wakati kulingana na aina ya wateja walionao kwa kuzingatia kanuni na sharia.
Afisa ustawi wa jamii Manispaa ya Morogoro Jasmin Kasenge amesema kikao hicho ni muhimu kwa maafisa ustawi wa jamii kwani kitawawezesha kuongeza ushirikiano na mshikamano miongoni mwao pamoja na ujuzi wa kufafanua miongozo mbalimbali ya utendaji kazi wao.
Nae Paul Fidelis ambae ni Afisa Ustawi wa jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ameiomba Jamii kutoficha watoto wanaonyanyaswa kisha kesi hizo kumalizana kindugui kwani kufanya hivyo ni kunyang’anya haki za watoto, na kuitaka jamii kuripoti matukio hayo kituo chochote cha Polisi kilicho karibu pindi yanapotokea.
Akiongea kwa niaba ya maafisa ustawi wa jamii waliohudhuria katika kikao hicho Afisa ustawi wa jamii kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa amesema wamepokea maelekezo waliopewa na Mgeni rasmi wa kikao hicho na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuboresha utoaji huduma kwa jamii.
Mkoa wa Morogoro una jumla ya maafisa ustawi wa jamii 35 ambapo Sekretarieti ya Mkoa yupo mmoja, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo wapo 3 huku maafisa ustawi wa Jamii 31 pekee ndio ambao wamegawanywa katika ngazi mbalimbali za Serikali za mitaa idadi ambayo bado haikidhi mahitaji .
MWISHO
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.