Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI inatarajia kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo ya Sekta ya Elimu Mkoani Morogoro inayotekelezwa chini ya mradi wa kuimarisha elimu ya Sekondari – SEQUIP na kuimarisha elimu ya Awali na Msingi – BOOST katika Halmashauri Nne za Mkoa huo.
Hayo yamebainishwa Februari 19, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima wakati akitoa taarifa ya miradi hiyo ambayo moja ya miradi itakayotembelewa ni Ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana Morogoro iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro DC.
Akitoa taarifa ya miradi hiyo Mkuu wa Mkoa huo amegusia changamoto ya Mradi wa Sekondari ya Wasichana ya Morogoro huku akiiomba Kamati hiyo ya Bunge kutupia jicho la pekee mradi huo kutokana na changamoto kubwa iliyopo katika utekelezaji wake mradi ambao unagharimu jumla shilingi Bil. 3.
“...hili la shule ya sekondari ya bilioni tatu…kuna kamati ya usimamizi lakini ule muundo mzima wa kusimamia ile hela ni jambo la ajabu sijawahi kuona…” amesema Mkuu wa Mkoa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Dennis Londo ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mikumi kwa niaba ya wajumbe wengine wa Kamati hiyo ameonesha dhamira yao ya kuitaka Serikali kudhibiti matumizi mabaya ya fedha zinazotokana na mapato ya Halmashauri kwa kuwa amesema fedha zinazotoka Serikali Kuu zinalemaza Halmashauri nyingi hapa nchini.
Aidha, Mwenyekiti huyo ameeleza kwa ufupi maazimio ya kamati hiyo ambayo yatajadiliwa kipindi cha Bajeti kuwa ni pamoja na masuala mtambuka kama suala la Lishe, taulo za kike, ukusanyaji na matumizi na mapato ya ndani, viwanja vya michezo na miundombinu ya shule kama vile vyoo, Madarasa na utoshelevu wa madawati.
Katika hatua nyingine, Mhe. Dennis Londo amempongeza Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Adam Kighoma Malima kwa ubunifu wake kwa kuzifanyia tathmini Halmashauri za Mkoa huo kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wao na kuimarisha usimamizi wa fedha za Serikali wanazokusanya katika Halmashauri zao na zile zinazopokelewa kutoka Serikali Kuu.
Kwa mujibu wa Ratiba iliyotolewa, Kamati hiyo itatembelea Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Mvomero, Kilosa, Ifakara na Halmashauri ya Mlimba kuanzia Februari 19 hadi Februari 24, 2024.
MWISHO.
Mvuha Area, Mvuha - Magogoni Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.