TAJIRI KIHEMBA, Moro Dc
Kamati ya fedha,uongozi na mipango ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro imefanya ziara yake ya kukagua miradi ikiwa ni ziara yake ya kukamilisha taarifa ya robo ya tatu kwa mwaka wa fedha wa 2020/2021.
Ziara hiyo imefanyika kwa siku mbili mfululizo kuanzia tarehe 3 Mei hadi 4 Mei mwaka 2021 ambapo wajumbe walipata fursa ya kutembelea ujenzi unaoendelea katika maeneo ya Shule ya Sekondari Mikese, Sekondari ya Nelson Mandela, Zahanati ya Mhunga Mkola, Sekondari ya Tomondo, Soko la Mkuyuni, Sekondari ya Matombo, Sekondari ya Mtombozi, Zahanati ya Lundi, Jengo la Utawala la Halmashauri (Mvuha) na Wodi za wanawake, wanaume na watoto katika Hospitali ya Wilaya.
Lakini pia Kamati ilipata fursa ya kukagua magari ya Halmashauri yanayoendelea na utengenezwaji katika karakana za Halmashauri na karakana nyingine TEMESA na TOYOTA ambapo Kamati kupitia Mwenyekiti wake ambae pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Lucas J. Lemomo imewataka wadau hao wafanye tathmini zao za mwisho na wawasilishe taarifa ya ubovu wa magari na gharama za utengenezaji ili Halmashauri ione zile gari zinazoweza kutengenezwa kwa haraka ziweze kutengenezwa na kuendelea kutumika katika shughuli za utekelezaji wa majukumu ya Halmashauri.
Katika hatua nyingine Mhe. Lucas J. Lemomo amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Bi. Rehema S. Bwasi kwa usimamizi mzuri wa miradi na kwa namna kasi ya utekelezaji wa miradi unavyokwenda haraka hasa ujenzi wa wodi za wanawake, wanaume na watoto katika Hospitali ya Wilaya unaotekelezwa kwa fedha kutoka Serikali kuu kiasi cha shilingi millioni mia tano pamoja na jengo la ofisi za Halmashauri ambao unatekelezwa baada ya kupokea fedha za awali kiasi cha shilingi millioni mia saba na hamsini.
“Kiukweli hili limenifurahisha niseme tu ukweli kasi mnayokwenda nayo ni nzuri na inaridhisha, niwaombe muongeze spidi zaidi tumalize kabla ya wakati sio lazima kumaliza ndan ya wakati tunaweza kumaliza kabla ya wakati” Mhe. Lucas J. Lemomo amesisitiza alipokuwa akikagua ujenzi wa wodi hizo tatu.
“Lakini pia sikutegemea kukuta hiki kinachoendelea katika eneo la ujenzi wa jengo la Utawala la Halmashauri kwani nilifikiri nitakuta mnasafisha eneo kumbe mmeshafikia hadi uchimbaji tayari kwa kunyanyua nguzo, nawapongeza sana muendelee na hii kasi” ameongezea Mhe. Lucas J. Lemomo wakati wa kukagua ujenzi wa jengo la utawala la Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
MWISHO.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.