Na Andrew Chimesela – Morogoro
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe amewataka wafanyakazi katika mashirika ya Umma na binafsi kutekeleza majukumu yao kikamirifu ili kuinua uchumi wa Mkoa badala ya kuendeleza porojo na mambo yasiyohusiana na kazi pindi wawapo kazini.
Dkt. Kebwe ameyasema hayo leo Mei Mosi akitoa hotuba yake kwa wafanyakazi ambao wako kwenye vyama mbalimbali vya wafanyakazi ikiwa ni maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani iliyofanyika kimkoa katika uwanja wa Jamhuri Mjini Morogoro Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro.
Amesema wafanyakazi wanapaswa kuwajibika kikamilifu kwani kufanya hivyo kutasaidia kuongeza pato la Mkoa na Taifa kwa jumla na hivyo kuwa rahisi kwa Serikali kufanya tathmini ya namna ya kuongeza kiwango cha mishahara kwa watumishi.
“Serikali haiwezi kuongeza mishahara kama hatutafanya kazi kwa tija ili kuongeza pato la Taifa kufanya hivyo ndio kutapelekea kupandisha kiwango cha mishahara kwa watumishi”. Alisema Dkt. Kebwe
Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka waajiri wa Sekta binafsi na mashirika mbalimbali ya umma kutoa michango ya wafanyakazi wao kwenye mifuko Pension kwa wakati pamoja na kuzingatia kiwango cha thamani ya pato linalozalishwa kulingana na viwango vilinavyokubalika na Serikali..
Awali akitambulisha wageni waliofika katika sherehe hiyo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Cliford Tandari amewataka wafanyakazi kuelewa kuwa haki na wajibu ni mambo yanayokwenda pamoja hivyo amewataka kutimiza wajibu wao kwanza ndipo wadai haki zao.
Kwa upande wake mwenyekiti wa vyama vya wafanyakazi Mkoa wa Morogoro (TUCTA) Mohammed Simbeye amemuomba Mkuu wa Mkoa kufuatilia kwa karibu mashirika yenye nia ya kuchafua jina la Mkoa huo kwa kuzuia haki za wafanyakazi ikiwemo kuanzisha vyama vyao wakiwa katika maeneo yao ya kazi.
Kupitia Risala iliyosomwa kwa Mgeni rasmi, wafanyakazi Mkoani humo wamemuomba Mkuu wa Mkoa kusaidia kuwasukuma waajiri katika Mashirika mbalimbali yaliyoko Mkoani Morogoro ili wasajiri wafanyakazi wao katika mifuko ya bima ya Afya bila kujali kipato anachopata mfanyakazi husika.
Sherehe ya siku ya wafanyakazi hufanyika kila ifikapo Mei Mosi ya kila mwaka ikiwa na lengo la kutathmini mwenendo na hali za wafanyakazi ikiwa sambamba na kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wafanyakazi ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni “Tanzania ya Uchumi wa Kati inawezekana, Wakati wa Mshahara na Maslshi Bora kwa Wafanyakazi ni SASA”.
Mvuha Area, Mvuha - Magogoni Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.