Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Loata Ole Sanare amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali Mkoani humo kushirikiana katika kutatua changamoto zinazowakabili wananchi ili kuwaletea maendeleo.
Sanare ameyasema hayo Januari 7, 2020 wakati akifunga kikao baina yake na watumishi wa ngazi ya Mkoa, Wabunge wa Mkoa huo, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kilichoandaliwa kwa lengo la kujadili kwa pamoja kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wa Mkoa huo na namna ya kuzitafutia ufumbuzi.
Sanare ameshangazwa na mwenendo wa baadhi ya wabunge wa mkoa huo wa kutoshiriki katika vikao muhimu vinavyoitishwa ngazi ya Mkoa akisema kwamba ndani ya vikao hivyo ndio sehemu wanayoweza kupata kero mbalimbali za wananchi wanaowaongoza na kuziwasilisha bungeni.
Kauli hiyo ya mkuu wa mkoa inakuja, ikiwa tayari ameshatembelea Halmashauri zote za Mkoa huo tangu kuripoti Mkoani humo sambamba na kushiriki katika vikao vikubwa vya kimkoa kikiwemo kile cha Bodi ya Barabara na Kikao cha ushauri cha Mkoa (RCC) huku idadi ya wabunge waliohudhuria ikiwa hairidhishi ukilinganisha na wabunge wote 14 waliopo Mkoani humo.
Ameongeza kuwa katika kutafuta ufumbuzi wa kero za wananchi yapo masuala yanayo hitaji ushiriki wa wabunge moja kwa moja katika utatuzi wake ukiachilia mbali masuala yanayo hitaji kusimamwa kisheria.
Washiriki wa mkutano huo wamepongeza maamuzi ya Mkuu wa Mkoa, wakisema pamoja kikao hicho kimekuja kwa kuchelewa kitasaidia kuweka dira ya mbeleni, ukizingatia viongozi wote kila mmoja ana nafasi yake katika kuwatumikia wananchi.
Kikao hicho cha siku moja, kimelenga kuwakutanisha wabunge wote wa Mkoa huu, Wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wajumbe wote wa kamati ya ulinzi na usalama, kuweka mikakati ya pamoja kutafuta ufumbuzi wa changamoto kwa wananchi, sambamba na taarifa ya maendeleo katika sekta ya elimu huku Mkuu wa Mkoa akisistiza kufanyika kwa kikaokama hicho kila baada ya kipindi cha robo mwaka kupita.
Na. Andrew Chimesela, Morogoro.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.