Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mh Loata Sanare amewataka wananchi wenye sifa wa mkoa wa Morogoro kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la kudumu la wapiga kura ili wapate fursa ya kuchagua viongozi wao katika uchaguzi wa Serikali za mitaa, unaotarajiwa kufanyika tarehe 24/11/2019.
Mhe. Sanare ametoa wito huo Oktoba 9 mwaka huu wakati akiongea na waandishi wa habari Ofisini kwake ikiwa ni siku moja tangu kuanza rasmi kwa zoezi hilo la uandikishaji wapiga kura.
Amesema zipo sababu nyingi zinazopelekea Serikali kuweka zoezi hilo ikiwemo kutoa fursa kwa wananchi waliotimiza Umri wa kupiga kura, waliohama miji au mitaa ya awali na waliopoteza vitambulisho vyao lengo likiwa ni kupata idadi kamili ya wakazi wenye sifa ya kupiga kura katika eneo husika.
“kuna mambo mengi yamepita hapa katikati, wapo watu wamehama mitaa na wengine wamefariki, hivyo ndio maana Serikali imeweka fursa hii ya kujiandikisha upya. Kwa hiyo wito wangu ni wananchi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha ili Serikali iwe na uhakika wa idadi ya wapiga kura waliopo katika vituo husika”, Alisema Sanare.
Katika hatua nyingine Mhe. Sanare amewataka wasimamizi wa uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa kutenda haki katika utekelezaji wao bila kumuonea mtu ili wapatikane viongozi waliochaguliwa na wananchi kihalali.
Akitoa raia hiyo amewataka wananchi nao watambue kuwa kura moja ya mwananchi ina uwezo wa kubadili matokeo ya uchaguzi mzima, na kumpata kiongozi wamtakaye au wasiyemtaka. Hivyo ni vema kila mwananchi ajiandikishe kwa ajili ya kuja kupiga kura.
Aidha Mkuu huyo wa Mkoa amesema jumla ya watu 1,423,111 wanatarajiwa kujiandikisha Mkoani Morogoro kupitia zoezi hilo ambapo katika siku ya kwanza ya zoezi wakazi 203,553 sawa na asilimia 14.30 walijiandikisha katika vituo mbalimbali.
Zoezi la kupiga kura kuchagua viongozi wa Serikali za mitaa mwaka huu, ambapo mitaa 327, vijiji 671 na vitongoji 3380 vinatarajia kushiriki uchaguzi kwa kuchagua wenyeviti wao,wajumbe wa kamati na wajumbe wa kamati maalumu wanawake.
Mvuha Area, Mvuha - Magogoni Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.