HALMASHAURI ya Wilaya ya Morogoro, katika mwaka wa fedha 2022/2023 imetenga Sh. milioni 30 kwa ajili ya kuanzisha Mradi ya Usimamizi Shirikishi wa Misitu (USMJ) katika vijiji vitatu vya Lumbachini, Sesenga na Lubumu.
Halmashauri hiyo inakuja na wazao hilo baada ya kuona mafanikio ya UMSJ katika vijiji vya Matuli, Lulongwe, Diguzi, Mlilingwa na Tununguo ambavyo vimeweza kutekeleza miradi ya maendeleo na jamii.
Wananchi wa Matuli wanatekeleza Mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS), maarufu ‘Mkaa Endelevu’ kupitia wa uwezeshaji wa Shirika la Uhifadhi wa Misitu ya Asili Tanzania (TFCG) na Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Uswis (SDC).
Akizungumzia na wananchi wa kijiji cha Matuli Mkurugenzi wa Halmashauri, Bi. Rehema Bwasi, amesema mafanikio ya kijiji na wananchi wa Matuli yanawasukuma kuongeza vijiji vipya ili kuchochea maendeleo.
“Tushatupa nduano, kazi yetu ni kwenda kuvua samaki. Tumefundishwa ujanja, basi jukumu letu ni kuhakikisha tunasambaza dhana hii. Hatutegemei mradi huu kufa bali mradi huu utawezesha kusihi kizazi na kizazi.
Sisi halmashauri tumetenga zaidi ya Sh.milioni 30 ili tuweze kuingiza vijiji vitatu vya Lumbachini, Sesenga na Lubumu kwa mwaka huu wa fedha. Tumeona sukari tumeipata Matuli, Diguzi, Lulongwe, Mlilingwa na Tununguo kina mmoja lazima ailambe ilia one utamu wake,” alisema.
Bwasi amesema halmashauri inatarajia kutenga fedha kila mwaka ili waweze kufikia vijiji vyote 149 hasa vile ambavyo vina misitu ya uhifadhi.
Mkurugenzi huyo alisema wamejipanga kuendeleza ushirikiano na TFCG na MJUMITA na wadau wote wa uhifadhi ili kuhakikisha vijiji vyote venye misitu ya asili inachochea maendeleo.
Ofisa Mtendaji wa kata ya Matuli Omary Chombo alisema USMJ katika kijiji hicho umefanikiwa kuingizia zaidi ya Sh.milioni 105 ambazo zimewezesha ujenzi wa miradi ya madarasa ya shule ya sekondari na msingi, nyumba ya mganga, zahanati, matundu ya choo.
Pia amesema kupitia mradi huo wameweza kumlipa mlinzi mshahara, kuchimba visima sita vya maji, kukopeshana, kukata Bima ya Afya (CHF) kaya 326 na nyingine.
Chombo alisema pia wametenga fedha kwa ajili ya sekretarieti ya kijiji, posho ya doria hali ambaho inachochea uhifadhi.
“Pia mradi wa TTCS umeboresha elimu na kuchangia ufaulu kuongezeka, hii ni kutokana na kuwepo makambi ambayo yanasaidia wanafunzi kupata chakula,” alisema.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Maliasili kijiji cha Matuli, Sadiki Kondo mradi wa TTCS umefanya mapinduzi makubwa ya kiuhifadhi, mazingira, uchumi na maendeleo kijijini kwao.
Kondo alisema msitu wa hifadhi wa kijiji cha Matuli una ukumbwa wa zaidi ya hekta 1,500 ambapo mradi unatekelezwa katika eneo la hekta 500 na kwa mwaka wanavuna vitalu 66.
“Mradi huu unafuata mzunguko wa miaka 24 baada ya kuvuna kitalu kimoja, hali ambayo kwa miti kama hii ya miombo inakuwa imeota tena kwa ajili ya uvunaji,” alisema.
Meneja Mradi wa Kuhifadhi Misitu kupitia Biashara Endelevu ya Mazao ya Misitu (CoFoReST), Charles Leonard alisema TFCG na MJUMITA wamelazimika kupeleka mpango wa USMJ ili kuokoa misitu ya vijiji kama sheria namba 5 ya ardhi ya 1999 inavyotaka.
“Misitu ya vijiji ilikuwa shamba la bibi, kwani kila mtu alikuwa anaingia anavuna, ila kupitia mradi huu, wananchi wamekuwa walinzi na wasimamizi wa rasilimali misitu, kwani wanapata faida nayo. Mradi unaisha Novemba mwaka huu naomba halmashauri ijipange kuendeleza,” alisema
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.