Katibu Tawala Mkoa wa Morogoro Dkt. Mussa Ali Mussa amesema mkoa wa Morogoro umejipanga kwa ajili ya kilimo cha mazao ya viungo hususani Karafuu ili kuongeza kipato cha Wananchi wa Mkoa huo na taifa kwa jumla sambamba na kurudisha uoto wa asili katika milima ya Urugulu.
Dkt. Mussa Ali Mussa ametoa kauli hiyo Januari 25, 2024 wakati wa kikao cha Wizara ya Kilimo cha kutambulisha mradi wa uzalishaji wa miche ya mikarafuu kilichofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Morogoro, kikao kilichoratibiwa kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo.
Amesema, kwa kushirikiana na mashirika mengine yakiwemo Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya usimamizi wa Wanyama Pori Tanzania (TAWA) watatoa bure kwa wananchi miche ya mazao ya Viungo ikiwemo miche ya mikarafuu ili waweze kupanda katika milima ya Uluguru zao litakalokuwa rafiki kwao na kusaidia kutunza mazingira ya milima hiyo.
"milima ya Uluguru inakabiliwa na uharibifu wa mazingira kwa kukata miti ovyo, kwa kupanda mazao hayo ya Karafuu itapelekea wananchi kutokata miti hiyo kwa kuwa inawaingizia kipato na wakati huo itahifadhi mazingira". Amesema Dkt. Mussa.
Katika Hatua nyingine Dkt. Mussa amesema kuwa, Mkoa huo umeanza kujenga maghala ya kuhifadhia karafuu ili kuwa na sehemu moja ya kuuzia zao hilo, na kusaidia Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kuweza kusimamia na kukusanya mapato yake vizuri.
Aidha, amesema, Wananchi wameweza kuhamasika na kuanza kupanda miche ya mikarafuu pamoja na kuzalisha miche hiyo si chini ya laki 4, hivyo kama mkoa wanajipanga ili kwenda kununua miche hiyo iliyozalishwa na wananchi na kuigawa kwao ili waipande.
Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Uzalishaji wa Mazao Wizara ya Kilimo Bi. Beatrice Banzi amesema lengo la kikao hicho inatokana na utafiti uliofanywa na Wizara hiyo siku za nyuma baada ya Mkoa wa Morogoro kuonesha nia ya kulima zao hilo.
Kwa sababu hiyo wizara ilifanya utafiti na kugundua kuwa sehemu kubwa ya Mkoa huo inaweza kustawisha zao la karafuu hivyo kuongeza kipato cha wananchi na kuhifadhi mazingira kwa sababu miti ya mikarafuu haifyonzi maji.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.