Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Bw. Ismail Ali Ussi, ameutaka uongozi wa Wilaya ya Morogoro kuhakikisha unatatua changamoto zilizopo katika soko la chakula la Ngerengere ili wananchi wa Ngerengere na wengine wanaolitumia soko hilo waweze kufanya biashara zao ndani ya soko hilo bila bughudha yoyote.
Bw. Ussi ametoa agizo hilo Aprili 11, 2025, wakati akikagua soko hilo ikiwa ni siku ya kwanza ya Mbio za Mwenge wa Uhuru kuwasili Mkoani Morogoro kwa ajili ya kuzindua, kuweka mawe ya msingi na kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo.
Amesema kuna umuhimu mkubwa kwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Mhe. Mussa Kilakala, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kushughulikia changamoto zote zinazolikabili soko hilo, zikiwemo miundombinu ya maji na vyoo, ili wafanyabiashara waweze kufanya kazi zao pasipo shida kwa maendeleo yao binafsi na ya taifa kwa ujumla.
“Kuna baadhi ya changamoto ambazo nimeziona katika soko hili; kabla hatujafika mkoa wa tano, marekebisho yafanyike na tupate taarifa,” amesema Bw. Ussi.
Aidha, amewataka wananchi wa Tarafa ya Ngerengere kutunza miundombinu iliyopo ndani ya soko hilo na kuitumia ipasavyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu, kwani serikali hutumia fedha nyingi kuijenga.
Katika hatua nyingine, Bw. Ussi amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inalenga kuboresha maisha ya Watanzania katika sekta mbalimbali, ikiwemo sekta ya afya na upatikanaji wa maji vijijini.
Pia, ameishukuru jamii ya Kata ya Mikese kwa kuwakaribisha wawekezaji, hususan mwekezaji wa mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme za zege kitakachogharimu zaidi ya shilingi bilioni 3.5 hadi kukamilika kwake, na ambacho kinatarajiwa kutoa ajira kwa wananchi wapatao 120 wa tarafa hiyo.
Ameongeza kuwa kiwanda hicho kitasaidia kupunguza changamoto ya nguzo zinazodondoka, hali inayosababisha kukatika kwa umeme mara kwa mara, na kuwataka wananchi kukitunza kiwanda hicho kwa manufaa yao na vizazi vijavyo.
Mbio za Mwenge wa Uhuru mkoani Morogoro, katika Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, zimetembelea jumla ya miradi nane yenye thamani ya shilingi bilioni 4.4. Mwisho wa mbio hizo ulihudhuriwa na Bw. Ussi ambaye alifunga kongamano la vijana lililofanyika kwa siku saba na kujikita katika mafunzo ya uzalendo, maadili mema, na ujasiriamali.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.