WAHESHIMIWA Madiwani wa Halmashauri ya Morogoro, wametakiwa kutambua kuwa ili kuwa na utawala bora wanao wajibu wa kushugulika na changamoto zinazowakabili wananchi kwa kuhakikisha vikao vya kisheria vinafanyika inavyostahiki kwani vikao hivyo ni njia mojawapo ya kushughulika na kero za wananchi lakini pia kujiletea maendeleo katika maeneo yao.
Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Mhe. Lucas Lemomo, wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Madiwani leo Januari 29/2021 katika Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri hiyo.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mhe.Lemomo, amewataka Madiwani kuhakikisha wanasoma kanuni za Halmashauri na taarifa mbalimbali zinazotoka kwa wataalam lakini pia kujenga ushirikiano katika kutatua kero mbalimbali pamoja na kutekeleza maagizo yote yanayotolewa na Serikali Kuu ili halmashauri iweze kwenda vizuri.
Aidha,Mhe.Lemomo,amewataka Madiwani kushirikiana na Halmashauri kuwa na mpango mkakati wa kuandaa master plan ya mji kwani shughuli mbalimbali zitaongeza kupitia ongezeko la watu kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi.
"Ndugu zangu dhamana tuliyopewa ni kubwa sana hamjatumwa huko halimashauri kwenda kujinufaisha sisi na familia zetu, twendeni tukayatekeleze yale tuliyoyaahidi ili kurudisha heshima tuliyopewa na wananchi, lazima tuwe kitu kimoja tufanye kazi kama timu na kuongeza vyanzo vya mapato ili tuboreshe miundombinu yetu bila kutegemea ruzuku kutoka Serikali Kuu " Amesema Mhe. Lemomo.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro , Mhe.Hamisi Msangule,amewata Madiwani pamoja na Watumishi wa Halmashauri kumpa ushirikiano wa kutosha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kusimamia makusanyo na matumizi ya fedha kutoka Serikali Kuu na Halmashauri ili kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mhe. Msangule,amesema kuwa dhamana na heshima waliyopewa madiwani na Wananchi ni kubwa mno na isiyoelezeka na jambo ambao anaweza kuahidi katika Baraza hilo ni ushirikiano wa kutosha katika kuleta maendeleo.
""Natambua uchaguzi huu ulioisha tulipitia mambo mengi sana ,lakini sasa uchaguzi umekwisha ni mwendo wa kuchapa kazi sasa twende kuchapa kazi ili turudishe ile heshima tuliyopewa na wananchi wetu kwa kutuchagua " Amesema Mhe.Msangule.
Mwisho, Mhe. Msangule, amemuomba Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na watendaji wote kuhakikisha wanashirikiana kwa ukaribu ili kuhakikisha wanatatua na kumaliza kero zote zinazowakabili wananchi.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Bi. Rehema Bwasi amesema kama viongozi wanao wajibu wa kuweka mazingira bora ya kujifunza kwa ajili ya kizazi Cha Sasa na baadae.
Naye Diwani wa Kata ya Mkambarani, Mhe. Chars Mbona,amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri, Wakuu wa Idara na Vitengo kwa usimamizi mzuri wa miradi kipindi ambacho Baraza la Madiwani lilivunjwa.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.