FAHAMU CHIMBUKO LA KAMPENI YA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA DUNIANI.
Kila mwaka kuanzia Novemba 25 hadi Desemba 10 Dunia hufanya kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia lengo likiwa ni kupinga ukatili na kutetea haki za wanawake.
Ukatili wa kijinsia ni kitendo chochote ambacho anaweza kutendewa mwanaume, mwanamke au mtoto na kitendo hicho huweza kumuathiri kimwili au kisaikolojia. Wanawake na watoto ndio wamekua wahanga wakubwa wa kufanyiwa ukatili wa kijinsia.
Toka mwaka 1981, wanaharakati wa haki za wanawake wamekua wakiitumia Novemba 25, kuadhamisha kupinga ukatili ili kuwaenzi wanaharakati wa kisiasa watatu (Mirabal Sisters) ambao waliuwawa mwaka 1960 huko Jamhuri ya Dominika mwaka 1960, kwa amri ya aliyekua kiongozi wa nchi hiyo Rafael Trujillo.
Mwaka 1993 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio la kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake kwa kuweka mikakati ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana..
Azimio hilo lilipelekea Baraza hilo mwaka 2000 kuweka azimio likitaja rasmi Novemba 25 kua ni Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake. Tamko hili lilipelekea serikali , pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi mbalimbali, kuunga nguvu za pamoja na kuandaa shughuli mbalimbali zenye lengo la kuufanya umma kuongeza ufahamu juu ya suala la kutokomeza ukatili wa kijinsia.
Mwaka 2006, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Awamu ya saba Ndugu Koffi Annan, alitaka Dunia itambue kua ukatili wa Kijinsia dhidi ya wanawake na watoto wa kike limekua tatizo kubwa hivyo aliona kuna haja ya kua na kipindi maalumu cha kampeni ya kupinga ukatili wa kijinsia. Hivyo ilikubalika kampeni hiyo ianze Novemba 25 ambayo ni Siku ya Kupinga Ukatili wa Kijinsia na kuhitimishwa Desemba 10 ambayo ni Siku ya Haki za Binadamu Duniani.
Lengo la kampeni hii ni kuongeza ushawishi, kubadilishana taarifa na uzoefu, kujenga uwezo wa pamoja, matumizi mazuri ya rasirimali zinazopatikana na kuunganisha nguvu za asasi za kijamii katika kuhamasisha, kuelimisha, kukemea na kuchukua hatua kwa pamoja ili kupinga ukatili wa kijinsia katika jamii.
Hivyo basi Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia inalenga kupaza sauti ili kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu athari hasi za ukatili wa kijinsia na njia za kuondokana na unyanyasaji huo katika jamii.
Serikali pamoja na wadau mbalimbali wanaotetea Haki za Binadamu, hufanya shughuli mbalimbali katika kampeni hiyo ikiwemo midahalo mbalimbali ya hadhara au kwenye taasisi kama vile shuleni na vyuoni
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.