Na. Andrew Chimesela, Morogoro
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anatarajia kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Mradi wa kufua umeme kupitia maporomoko ya maji ya mto Rufiji ikiwa ni ishara ya uzinduzi rasmi wa ujenzi wa Mradi huo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 24 katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Waziri wa Nishati Mhe. Merdadi Kalemani amesema uwekaji wa jiwe la msingi unatarajiwa kufanyika siku ya Ijumaa tarehe 26 Mwezi huu katika eneo la mradi huo ambapo Rais Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.
Amesema utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuwa na manufaa makubwa katika adhma ya kuipeleka nchi katika uchumi wa kati ambao unategemea kwa kiasi kikubwa uwepo wa nishati ya kutosha hususani katika shughuli za viwandani.
Ameongeza kuwa mradi huo utakaogharimu kiasi cha fedha shillingi Trilioni 6.5 hadi kukamilika kwake unatarajia kuzalisha Megawati 2115 kiwango ambacho kitakidhi mahitaji ya ujenzi wa uchumi wa viwanda huku ukitarajiwa kukamilika mwaka 2022.
Aidha Waziri Kalemani amesema Tayari mradi huo umeshatumia muda wa miezi saba ya utekelezaji wake tangu ulipoanza mnamo mwezi Disemba mwaka jana ambapo maendeleo yake ni ya kuridhisa hivyo uwekaji wa jiwe la msingi utachochea kasi ya ujenzi wake.
Amesema Mkandarasi wa ujenzi huo alianza kazi rasmi mwezi juni mwaka huu ambapo kwa sasa kazi mbalimbali zinaendelea ikiwemo kuchoronga miamba pamoja na ujenzi wa madaraja katika eneo la mradi.
Amebainisha kwamba mradi huo utakuwa mwarobaini wa kupunguza uharibifu wa mazingira unaotokana na matumizi ya kuni na mkaa ambapo mikoa ya Pwani, Morogoro na Iringa imekuwa ikizalizalisha kiwango cha mkaa unaotokana na ukataji wa miti hivyo kuharibu sehemu kubwa ya uoto wa asili.
Awali akimkaribisha Waziri wa Nishati, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt. Kebwe Stephen Kebwe amesema tayari vijiji 22 vimeshanufaika katika kipindi hiki cha ujenzi wa mradi huo kwa kuunganishiwa umeme jambo ambalo halikuwa rahisi hapo kabla.
Aidha amewataka wakazi wa Mkoa wa Morogoro kuchangamkia fursa ya ujenzi wa mradi huo kujikwamua kiuchumi kupitia ajira za watu zaidi ya elfu 10 zitakazozalishwa kutokana na mradi huo .
Mradi wa kufua umeme kupitia maporomoko ya maji ya mto Rufiji unatarajiwa kuwa miongoni mwa miradi mikubwa ya kufua umeme Duniani ambapo kwa bara la Afrika utatarajiwa kushika nafasi ya nne ambapo utaambatana na ujenzi wa bwawa lenye ujazo wa mita za ujazo billion 532 ambalo litashika nafasi 60 kati ya mabwawa makubwa 70 duniani ambapo shillingi Trilioni 6.5 zinatarajiwa kutumika mpaka kukamilika kwake mnamo mwaka 2022.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.