Na Andrew Chimesela - Morogoro
Licha ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mkuyuni Mkoani Morogoro kuchukua muda mrefu kakamilika, Katibu Tawala wa Mkoa huo Mhandisi Emmanuel Kalobelo amefurahishwa na hatua ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro katika kukamilisha baadhi ya majengo ya kituo hicho na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Mhandisi Kalobelo ametoa pongezi hizo Juni 4 mwaka huu alipofanya ziara ya kukagua na kuhimiza ujenzi wa vitio vya Afya vya Mkuyuni, Kisemo, Kisaki na Hospitali ya Wilaya akiwa ameambatana na baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Mkoa na kushuhudia miradi mingi iko katika hatua za umaliziaji.
Katibu Tawala wa Mkoa Morogoro Mhandisi Emmanuel Kalobelo (kulia) pamoja na msafara wake wakiangalia shimo la maji taka katika kituo cha Afya cha Kisemo Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro.
Kwa mujibu wa Katibu Tawala, ziara hiyo ililenga kujiridhisha utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa wakati wa kikao cha madiwani wa Halmashauri hiyo cha kupitia hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kilichoagiza kukamilisha miradi hiyo mapema, lakini pia kuangalia utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa wakati wa ziara yake aliyoifanya mwanzoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Baadhi ya majengo ya Kituo cha Afya cha Mkuyuni
Ziara hiyo pia ilikuwa na lengo la kujiridhisha ujenzi wa Kituo cha afya cha Kisaki ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli alitoa ahadi kwa wananchi akiwa njiani kwenda kuweka jiwe la Msingi mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere.
Katibu Tawala Mhandisi Emmanuel Kalobelo (kushoto) akikagua ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kisaki
Aidha, ziara hiyo ilikuwa na lengo la kumpitisha kwenye miradi ya maendeleo ya halmashauri hiyo, Mkuu wa Wilaya Mpya wa Wilaya ya Morogoro Bakari Msullwa na kumfahamisha baadhi ya changamoto za miradi hiyo ili aweze kushirikiana na Serikali ngazi ya Mkoa katika kuzitatua.
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bakari Msullwa (katikati) akisikiliza kwa makini maelekezo ya Mhandisi Kalobelo anayoyatoa kwa baadhi ya wajumbe wa Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro (hawapo pichani) katika kukamilisha ujenzi wa kituo cha Afya Kisemo
Kuhusu Kituo cha Afya cha Mkuyuni, Mhandisi Kalobelo ameipongeza Halmashauri hiyo kukamilisha baadhi ya majengo na kuanza kutoa huduma kwa wananchi huku yeye akishuhudia akina mama waliojifungulia Kituoni hapo wakiwa na furaha tele ambapo Bi. Fatma Seleman kwa niaba ya wenzake alimshukuru Rais John Pombe Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya.
“lakini cha kufurahishwa wote tumeona pamoja, kituo kile sasa kimeanza kutoa huduma akina mama wanajifungulia pale na wamefurahi” alisema Mhandisi Kalobelo.
Mhandisi Kalobelo (kushoto) na Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bakari Msullwa (kulia) wakimjulia hali mmoja wa akina mama waliojifungulia kwenye majengo mapya ya Kituo cha Afya cha Mkuyuni
Hata hivyo, Kalobelo aliwataka Viongozi wa Halmashauri ya morogoro kukamilisha kazi zilizobaki ikiwa ni pamoja na kufunga vifaa tiba, uingizaji wa maji, usafi wa mazingira ya nje na kukarabati majengo ya awali yafanane na majengo mapya.
Katika hatua nyingine Mhandisi Kalobelo amewapongeza Manesi wanaofanya kazi kituo cha Afya cha Mkuyuni kwa kufanya kazi kwa upendo kwa wagonjwa. Hii ni baada ya manesi hao kupongezwa na akina mama waliojifungulia katika kituoni hapo kuwapongeza wahudumu hao mbele ya Mhandisi Kalobelo.
“tunashukuru hapa tumetembelea akina mama ambao wamejifungua hapa kwamba manesi wanawahudumia vizuri, hii kauli mara chache sana kuisikia…kwanza niwapongeze manesi wanaofanya kazi hapa jinsi wanavyowahudumia akina mama na wagonjwa wengine wote sababu ni nadra sana kupata sifa ya namna hii” Kalobelo alipongeza.
Akiwa katika eneo la Hospitali ya Wilaya hiyo, Mhandisi Kalobelo pamoja na msafara wake hawakuridhishwa na ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kisemo na Hospitali ya Wilaya hiyo kwa sababu ya kasi ndogo ya ujenzi inayoendelea huku miradi hiyo ikiwa na fedha ikiwemo Hospitali kiasi cha shilingi 535Mil. na Kituo cha Afya Kisemo kikiwa na shililingi Mil. 64.
Akihitimisha ziara hiyo katika kituo cha Afya cha Kisaki, pamoja na changamoto zote zilizopo katika ujenzi wa kituo hicho Mhandisi Kalobelo ameagiza kituo hicho kikamilike kabla ama ifikapo Mwenzi Septemba mwaka huu.
Aidha amesema, katika miradi yote inayojengwa wilayani humo jambo la msingi linalotakiwa kuwa na tahadhari ni kukamilisha kazi hizo kwa wakati ikiwa na ubora unaohitajika lakini zaidi kazi zinazofanywa zilingane na thamani ya fedha iliyotumika kwa kila mradi husika.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Bakari Msulwa pamoja na kuahidi kuyasimamia maagizo ya Katibu Tawala, amewataka watumishi wa Halmashauri hiyo kuacha visingizio katika utendaji wao wa kazi na atakayeonesha kuwa ni kikwazo atapendekeza mtumishi huyo kuondolewa katika halmashauri hiyo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Rehema Bwasi, ameema Halmashauri yake imefanya jitihada za dhati katika kupata fedha shilingi milioni 200 kwa ajili ya kumalizia majengo ya kipaumbele ya Hospiatali ya Wilaya. Hata hivyo ameahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wakati wa Ziara hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Rehema Bwasi (wa pili kushoto) akiwa na mgeni wake Mhandisi Kalobelo wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo
Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ni moja ya halmashauri chache hapa nchini zilizobahatika kupata fedha nyingi za kujenga Vituo vya Afya ambapo hadi sasa imepewa fedha za kujenga vituo vya Afya sita (6) pamoja na Hospitali ya Wilaya.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.