Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Mussa Kilakala, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Adam Kighoma Malima, ameongoza maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Kisaki Gomero, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, tarehe 10 Septemba 2025.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na mamia ya wazee kutoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Morogoro ambapo pamoja na kupewa nafasi ya kushiriki kwenye sherehe hizo, walipata huduma za afya bure ikiwemo vipimo vya presha, kisukari, ushauri wa lishe na huduma za uchunguzi wa macho.
Katika hotuba yake, Mhe. Kilakala aliwataka wananchi wote kuendelea kuthamini, kuheshimu na kuwajali wazee kwa kuwa ni hazina ya busara na maarifa katika jamii. Alisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuboresha huduma za kijamii kwa wazee, ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa huduma za afya bila malipo kwa wazee wote wenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea.
Baada ya sherehe hizo, wazee walipata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Mwalimu Nyerere na Bwawa la kuzalisha umeme Kwa nguvu ya Maji la Mwalimu Nyerere (JNHP) – ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wao kwa Taifa na kuwapatia muda wa mapumziko ya kijamii na kielimu.
Maadhimisho hayo yaliambatana pia na burudani mbalimbali zikiwemo ngoma za asili, maigizo na mashairi ya kuenzi mchango wa wazee katika maendeleo ya jamii.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni "Wazee ni Nguzo ya Maendeleo – Tuwaenzi, Tuwaheshimu na Kuwatambua."
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.