“Misitu ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya nchi ambayo inahitaji ushirikiano wa kutosha katika kuhakikisha inakuwa endelevu hivyo ipo haja ya jamii kushirikishwa kwa kiasi kikubwa ili kuhakikisha inatunzwa na kutumika katika hali ya uendelevu ili kuleta matokeo chanya.”
Hayo yamebainishwa na Meneja mradi wa Mkaa endelevu unaotekelezwa na Shirika la kuhifadhi Misitu ya asili (TFCG) Bw. Charles Leonard ambapo amesema Tanzania ina hekta 48.1 za misitu hivyo ni vema ikatumika nguvu ya ziada kwa jamii katika kuielemisha na kujenga uelewa namna ya kuhifadhi, kutunza na kutumia misitu katika hali ya uendelevu kwani jamii ikielimika na kupata uelewa mtazamo wao utabadilika kuhusu kulinda, kutunza na kutumia rasilimali misitu.
Aidha kwa upande wa maafisa habari na mawasiliano kutoka serikalini na mashirika yasiyo ya kiserikali walioshiriki ziara ya kujenga uelewa juu ya mradi wa Kuleta Mageuzi katika Sekta ya Mkaa Tanzania (TTCS) wamesema mradi huo umetekeleza dhana ya uendelevu wa misitu ya vijiji na kulinda mazingira ambapo mkoani Morogoro unatekelezwa katika Halmashauri za Wilaya za Kilosa, Mvomero na Morogoro katika vijiji 35 huku wakisema kuwa ipo haja ya mradi huo kufanyika na kuendelezwa nchi nzima kwani una manufaa kwa nchi na wananchi kiujumla.
Pamoja na hayo wamesema kuwa kupitia ziara hiyo wamejifunza namna mradi huo unavyochochea utunzwaji wa mazingira na kuinua kipato cha wananchi huku wakisema kuwa endapo Serikali kwa kushirikiana na wananchi watatunza misitu hiyo itasaidia katika miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa nyumba za watumishi, ujenzi wa vituo vya afya na zahanati, upatikanaji wa madawati na mbao kwa matumizi mbalimbali jambo litakalosaidia kuepusha matumizi makubwa ya fedha kwa ajili ya ununuzi wa rasilimali za misitu kwa ajili ya miradi ya maendeleo.
Katika hatua nyingine akitoa taarifa fupi ya faida ya mradi wa Mkaa endelevu katika kijiji cha Kitunduweta, Afisa Mtendaji wa Kijiji Ndugu Thomas Lukoo amesema, “Kijiji cha Kitunduweka kwa mwaka tunavuna vitaru 83 sawa na gunia 6,640 ambapo kwa mwaka wa kwanza tulipata Tsh. 28,328,095/= na mwaka 2018/2019 tulipata Tsh. 27,128,095/= na mwaka 2019/2020 tulipata Tsh. 28,143,255/= lakini pia kupitia mradi huu tumeweza kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo kama kuwakatia wananchi Bima ya Afya ya CHF takribani Kaya 378, lakini pia tumefanya ukarabati wa madarasa ya shule ya msingi Kitunduweta, lakini pia tumemalizia nyumba ya mwalimu mkuu pamoja na kujenga choo cha kisasa cha nyumba ya mwalimu na pia tumetengeneza madawati kwa ajili ya shule yetu.”
Ziara hiyo ilimehudhuliwa na Maafisa Habari Serikalini kutoka taasisi mbalibali, wizara na Halmashauri za Morogoro, Kilosa, Mvomero na Kilolo ambapo ilitoa fursa kwa Maafisa hao kujifunza kuhusu mradi wa mkaa endelevu unavyofanya kazi lakini pia wamepaata fursa ya kubadirishana uzoefu katika maswala ya utoaji wa habari hasa katika maswala ya uhifadhi wa misitu.
#KAZIIENDELEE
Mvuha Area, Mvuha - Magogoni Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.