Na. TAJIRI KIHEMBA, Moro Dc
Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro imefanya kikao chake cha Baraza la Madiwani cha Robo ya tatu tarehe 12 Mei, 2021 katika ukumbi wa Pangawe na kujadili mambo mbalimbali kwa mstakabali wa Halmashauri.
Kikao hicho pia kilipata kuhudhuriwa na wageni mbalimbali waalikwa akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Bakari Msulwa, Katibu Tawala wa Wilaya ya Morogoro Bi. Ruth John lakini pia Msaidizi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Ndugu Francis G. Francis kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro.
Akimkaribisha Mwenyekiti wa Halmashauri kufungua kikao, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Bi. Rehema S. Bwasi amewashukuru Wakuu wa Idara na Vitengo, Maafisa Tarafa na Wageni waalikwa wote kwa kuudhuria kikao hiki adhimu ambacho kilikuwa kinakwenda kujadili mambo muhimu kwa mstakabali wa Halmashauri ya Wilaya ya Mororgoro.
Akitoa nasaha zake Mkuu wa Wilaya ya Morogoro Mhe. Bakari Msulwa amesema, “Makusanyo yetu bado si ya kutosha lakini nimefurahi tumekuwa tukikaa na Mheshimiwa Mwenyekiti na Mkurugenzi wamezungumzia habari ya kuwa na vyanzo vingine vya mapato, mimi niwaombe sana waheshimiwa madiwani mkitaka mfanikiwe nafikiri maneno mengi na kelele nyingi na mipango mingi ielekezwe kwenye vyanzo vya mapato.”
Lakini pia Mhe. Bakari Msulwa amezungumzia kuhusu Halmashauri kuwekeza katika kutoa Wanasayansi, “Kuna fedha zimetengwa takribani Shillingi mia tatu na sitini millioni zinakwenda katika shule kumi na mbili au kumi na tano hivi, mimi naomba ndugu zangu Waheshimiwa Madiwani tusimamie hili swala na katika eneo ambalo litatuvuruga huko mbele ya safari nimeshaongea na wakurugenzi, mawaziri na baadhi wa viongozi wa Serikali wanataka kufanya ziara ya kufuatilia hayo mambo. Tuhakikishe kuwa hizo fedha zilizotengwa katika maeneo yetu zinafanya kazi, tuwasimamie watendaji, tupige kelele kama kuna haja ya kupiga kelele lakini kubwa zaidi tuhakikishe maabala zetu zinafanya kazi ili sasa kutengeneza mazingira ya vijana wetu kuingia katika mkondo wa sayansi, haitapendeza miaka kumi au ishirini ijayo tunapima matokeo hatuna wanasayansi kutoka katika maeneo yetu kitakuwa ni kitu cha aibu sana, wanasayansi tunawatengeneza ndani ya ukumbi huu. Tukiamua kutengeneza wanasayansi tukiamua kutengeneza wasomi tukitengeneza hatima ya Halmashauri yetu ni sisi tumepewa jukumu mimi naamini timu hii inatosha kuifanya kazi hiyo.”
Kwa upande wa mwakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Msaidizi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro ndugu, Francis G. Francis amesema, “Sisi kama Mkoa kwanza tunawasifu ninyi Waheshimiwa Madiwani kwa utendaji mzuri ambao unatendeka sasa hivi, sisi kama ofisi ya Katibu Tawala tulikwenda katika Halmashauri yenu kutizama tatizo la minada nafikiri mna utaratibu mpya wa kuendesha minada katika Halmashauri yenu, tumepita katika Kata ya Duthumi, Tununguo, Mnada wa Diguzi, tumepita na tumeona lakini kwa kuwa utaratibu huo mpya ulikuwa bado haujaanza vizuri tumeshindwa kushauri vizuri sana lakini tunaamini kwamba huenda huo utaratibu mpya mkiusimamia vizuri unaweza ukawa mzuri. Kwa hiyo tunachokisema kwenu ni kwamba muongozo uwepo wa kuendesha huo utaratibu mpya.”
Ndugu Francis G. Francis ameongezea kwa kusema, “Sisi kama Mkoa tumeona tulizungumzie hapa kwani tunaamini lilianzia hapa kwenye Baraza lenu na mkaenda Chalinze kujifunza na sisi tukawasilisha kwa Katibu Tawala kwamba utaratibu unaweza ukawa mzuri ila kitu ambacho tulikiona pungufu kidogo, mnada kama ule unatakiwa uendeshwe chini ya uangalizi wa Polisi kiusalama, kwa hiyo kwa wiki hizi tatu ambazo minada hii imeendeshwa kwa utaratibu mpya Polisi ambao tuliwakuta kule wameenda lakini kulikuwa na utaratibu ambao haukuonyesha kwamba watakuwa sehemu ya malipo, hivyo sisi kama Mkoa tunashauri Polisi wale walipwe na Halmashauri.”
Mwisho Mwenyekiti wa Halmashauri, Mhe. Lucas J. Lemomo ameishukuru Serikali kuu, “Kwa namna ya pekee kabisa niishukuru Serikali Kuu na hasa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia Waziri wa TAMISEMI na timu yake yote ya Wizara kwa jinsi ambavyo wameweza kutuletea fedha ya ziada zaidi ya ile bajeti yetu kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, changamoto tunayokutana nayo katika fedha hizi zinazokuja nje ya bajeti ni vifungu vya kutuwezesha kutumia hizi fedha, hivyo tunaomba Wizara ya TAMISEMI kupitia kwa Waziri husika watusaidie kutanua vifungu ili tuweze kukamilisha miradi yetu kabla ya mwaka wa fedha kuisha.”
MWISHO.
Mvuha Area, Mvuha - Magogoni Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.