Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro leo Septemba 4,2025 imezindua rasmi zoezi la chanjo na utambuzi wa mifugo, likiwa na lengo la kuboresha afya ya mifugo na kuongeza thamani ya uzalishaji kwa wafugaji. Mgeni rasmi katika uzinduzi huo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Musa Kilakala, ambaye ameipongeza Halmashauri kwa kuandaa mpango huo muhimu unaogusa maisha ya wananchi wengi.
Katika hotuba yake, Mhe.Kilakala amesema serikali itaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha mifugo inalindwa dhidi ya magonjwa hatarishi, sambamba na kuimarisha mfumo wa utambuzi ili kudhibiti migogoro ya mifugo.
"Wote tunafahamu tunazo changamoto katika Wilaya yetu ya Morogoro hususani Halmashauri yetu ya Wilaya ya Morogoro, lakini Kwa kupitia jambo hili la utambuzi tunaweza kutatua changamoto hii Kwa kiwango kikubwa"Amesema Mhe.Kilakala
Aidha, amewataka wafugaji wote kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo mifugo yao inapatiwa huduma ya chanjo na kusajiliwa kwa mujibu wa utaratibu pia amewataka kuzingatia suala la ulinzi na usalama Kwa kuepuka migogoro kati ya Wafugaji na Wakulima.
Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Mhandisi.Magreth Kavaro , amesema Halmashauri imepokea kutoka Serikali kuu chanjo ya homa ya mapafu 130,000. Chanjo ya Sotoka Kwa Mbuzi na Kondoo 150,000. Chanjo ya Kideli,Mafua na Ndui Kwa Mifugo Jamii ya Kuku 150,000 .
Ameongeza Kwa kusema zoezi hilo linatekelezwa kwa kushirikiana na wataalamu wa mifugo wa Halmashauri ya Wilaya, na litasaidia kuweka takwimu sahihi za mifugo, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza mapato ya wananchi.
Kwa upande wa Wafugaji waliohudhuria uzinduzi huo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wafugaji Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro Ndg Kianjo Nyerera wameishukuru serikali kwa hatua hiyo, wakieleza kuwaa itaongeza uelewa na kuimarisha ufugaji wa kisasa unaowasaidia kujikwamua kiuchumi.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.