Na. Andrew Chimesela - Morogoro.
Wakurugenzi wa Halmashauri Mkoa wa Morogoro wametakiwa kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya shule yakiwemo madarasa kabla au ifikapo Januari 28 mwakani ili kuwafanya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza kuwa na mazingira bora ya kusomea.
Hayo yamefahamika wakati wa kikao cha Uchaguzi wa wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na Kidato cha kwanza Januari 2019 kilichofanyika katika Ukumbi wa Chuo cha Ualimu cha Morogoro ambacho pia kilihudhuriwa na wadau mbalimbali wa Sekta ya Elimu.
Muda mfupi kabla ya kutangaza matokeo ya uchaguzi huo, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro Bw. Ernest Mkongo alisema wanafunzi waliosajiliwa kufanya mtihani mwaka huu walikuwa 48,301 lakini waliofanya mtihani ni 47,961 sawa na asilimi 99.
Kwa mantiki hiyo, Kaimu Katibu Tawala huyo wa Mkoa ambaye pia ni Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji Mali ameagiza kila Halmashauri ndani ya Mkoa wa Morogoro kwenda kutathmini matokeo hayo na kupanga mikakati ya kuwapokea wanafunzi hao na kuwatayarishia mazingira ikiwa ni pamoja na kukamilisha ujenzi wa madarasa.
Amesema ifikapo Januari 28, 2019 majengo yote ya shule za Sekondari yanayojengwa au kukarabatiwa kwa kila Halmashauri Mkoani humo yawe yamekamilika bila visingizio vyovyote, lengo ni kuendelea kuboresha mazingira ya kujifunzia na wanafunzi waliofaulu ambao hawataripoti wazazi wao wachukuliwe hatua za kisheria.
“Hatutapokea visingizio vya aina yoyote kwa wanafunzi wasioripoti shuleni, hatua za kisheria zichukuliwe kwa wazazi au walezi watakaokwamisha wanafunzi hawa kuendelea na masomo yao” alisema Bw. Mkongo.
Naye Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. George Jidamva pamoja na kuupongeza Mkoa kwa kuwa na ufaulu mzuri ameagiza kuwasimamia Waratibu wa Elimu ngazi ya Kata kusimamia vema majukumu yao ili Mkoa uendelee kupata ufaulu mzuri zaidi .
Amesema kwa sasa Watendaji hao hawana kisingizio chochote kwa kuwa Serikali imekwisha wapatia usafiri wa pikipiki kwa ajili ya kuwasaidia kusimamia vema majukumu yao hivyo ni vema watendaji hao wakatumia vema usafiri waliopewa kwa manufaa ya kazi zao na Taifa kwa ujumla.
Hata hivyo Dkt. Jidamva amekumbusha kuendelea kusimamia uwepo wa chakula cha wanafunzi shuleni, kukamilisha ujenzi wa madarasa yatakayopelekea wanafunzi kupata masomo yao katika mazingira yaliyobora.
Kwa upande wake Afisa Elimu Mkoa wa Morogoro Mhandisi Joyce Baravuga amebainisha kuwa Mkoa wa Morogoro umepanda ufaulu kwa asilimia 6.6 ambapo mwaka 2017 ufaulu ulikuwa 70.78 na mwaka huu ufaulu umepanda hadi kufikia 77.38 wastani huo unatokana na kupanda kwa ufaulu kwa Halmashauri 8 kati ya 9 za Mkoa wa Morogoro ambapo Halmashauri moja tu ya Gairo ndiyo iliyoshuka kwa ufaulu kwa asilimia 5.73.
Mkoa wa Morogoro umefanikiwa kutoa mwanafunzi wa pili kitaifa INNOCENT PAUL SELELI kutoka shule ya Msingi Carmel katika Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro na hivyo mwanafunzi huyo kuwa miongoni mwa wanafunzi kumi bora kitaifa.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.