Wazazi na walezi wenye watoto chini ya umri wa miaka mitano wa kijiji cha Muungano kata ya Lundi halmashauri ya wilaya ya Morogoro wamepewa elimu ya afya,ikiwa ni utayarishaji, upishi wa vyakula na ulishaji kwa watoto wachanga na watoto wadogo kwa kuzingatia aina ya vyakula ambavyo watoto wanapaswa kula. lengo la elimu hiyo ni kuimarisha ukuaji, maendeleo na Afya ya mtoto.
Hayo yalijiri wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji (SALiKi) katika kijiji hicho yaliyofanyika Septemba 23, 2024 ambapo watu mbalimbali walishiriki ikiwa ni pamoja na wazazi/walezi wenye watoto chini ya miaka mitano, viongozi wa kijiji, wahudumu wa afya ngazi ya jamii na watumishi kutoka Hospital ya Wilaya.
Shughuli mbalimbali zilifanyika ikiwa ni pamoja na utoaji wa elimu ya Lishe, elimu ya Afya na umuhimu wa chanjo pamoja na kupima hali ya Lishe na kutoa chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano. . Aidha, wazazi na walezi walioshiriki walipata elimu ya uandaaji wa chakula cha watoto kwa njia ya mapishi kwa vitendo yaliyoongozwa na wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii.
Akitoa eimu ta lishe mhudumu wa afya bgazi ya jamii Bw. Msafiri Ngomeka amewasisitiza wazazi/walezi kuwapa watoto chakula ambacho ni mlo kamili kwa kuzingatia makundi ya vyakula ambayo ni nafaka, mizizi,ndizi mbichi kwa ajili ya kuupatia mwili wa mtoto nishati lishe (Wanga ) au nguvu, vyakula vya asili ya wanyama na vyakula vya jamii ya kunde ambavyo huupatia mwili protini kwa ajili ya ukuaji na kujenga afya njema, mbogamboga na matunda kwa ajili ya kupata vitamini na madini ambayo humkinga mtoto na maradhi na kuwezesha mwili wa mtoto kufanya kazi kwa ufanisi. Pia amesisitiza ni muhimu kuhakikisha wazazi wanawapa vyakula mchanganyiko kwa kuzingatia na kutumia vyakula vinavyopatikana katika mazingira yetu ambavyo ni rahisi na sio gharama
Sambamba na hayo watoto takribani 70 wamepimwa hali ya lishe (uzito kwa umri) na hakuna aliyekutwa na changamoto ya uzito pungufu.
Aidha watoto chini ya miaka mitano wamepatiwa dawa za minyoo na vitamini A. Ambapo watoto jumla ya watoto 14 walipata chanjo watoto 46 wenye umri kuanzia mwaka 1-5 walipatiwa vitamini A na dawa za minyoo.
Wananchi wa Lundi wameshukuru kwa kupatiwa elimu na hamasa ya uzingatiaji wa lishe bora haswa wakikumbushwa kuwa makundi yote saba ya vyakula vikiwepo na vile vya asili vinapatikana kwa urahisi katika maeneo yao.
Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji (SALiKi) ni siku maalum inayoadhimishwa mara moja kila robo ya mwaka katika ngazi ya kijiji kwa lengo la kuhamasisha masuala ya afya na lishe. siku hii ni mpango jumuishi wa kuboresha upatikanaji wa huduma za afya na lishe kwa mama na mtoto katika ngazi ya jamii, na utekezaji wake ni mojawapo ya afua maalum inayoweza kuchangia kupunguza matatizo ya lishe duni kwa watoto wachanga na jamii.
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.