Na. Tajiri Kihemba, MOROGORO DC.
Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro imezindua zoezi la upimaji wa viwanja katika Kijiji cha Kisaki Kituoni ikiwa ni hatua ya utekelezaji wa Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi katika Miji katika Halmashari ya Wilaya ya Morogoro.
Uzinduzi huo umefanyika jana Februari 24, 2022 na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Mhe. Lukas J Lemomo kwenye Mkutano wa Wananchi kijijini hapo.
Akizungumzia lengo la Serikali katika kupanga na kupima eneo la Kisaki, Mkuu wa Idara ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Ndugu Patrick Mwakilili amesema kuwa Serikali ina lengo la kuwezesha ukuaji endelevu wa makazi na shughuli za kiuchumi zitakazochochewa na mradi wa Bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Nyerere.
Viwanja 3,888 vya matumizi mbalimbali vinatarajiwa kupimwa na mradi huu unalenga makundi yafuatayo;
1. Wananchi wa kawaida kwa ajili ya kupata viwanja vya kujenga nyumba bora za makazi.
2. Wafanyabiashara kwa ajili ya kuweka biashara mbalimbali kama maduka, nyumba za kulala wageni na nyinginezo.
3. Wawekezaji kwa ajili ya kupata viwanja vya matumizi ya viwanda vidogo, hotel, kambi za kitalii, Elimu na uwekezaji mwingine.
4. Taasisi mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi.
Upimaji uliridhiwa na kupata Baraka za Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro ufanyike upimaji shirikishi wa viwanja kwa awamu kwa kugawana viwanja na wamiliki wa maeneo kwa uwiano wa asilimia 60 (Mwananchi) kwa asilimia 40 (Halmashauri ya Wilaya).
Asilimia 40 ya ardhi inayokwenda Halmashauri ya Wilaya ndio gharama ya kupima maeneo na kuweka miundombinu muhimu kama barabara, makaravati na miundombinu mingine ikiwa ni pamoja na kurudisha Mkopo wa fedha ambayo Halmashauri imekopa kwa ajili ya upimaji wa viwanja hivyo.
Kwa kuanzia, Halmashauri itapima viwanja 2,500 kwa kutumia makampuni ya upimaji ili kuharakisha upimaji na upimaji huo utaendelea kwa awamu hadi hapo eneo lote lililopangwa litakapopimwa lote.
Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro inatarajia kutangaza bei ya viwanja hivyo muda mchache baada ya kukamilika kwa zoezi la upimaji.
#KisakiNaNgerengereKuwaMijimidogo
Mvuha Area, 450M- Bigwa-Kisaki Road
Sanduku la barua: 1880, Morogoro Tanzania
Simu: +255 23 2935458
Simu ya Kiganjani:
Barua pepe: ded@morogorodc.go.tz
Hakimiliki ©2017 H/W Morogoro. Haki zote zimehifadhiwa.